6

Toba isiyo ya kweli
1 “‘Twendeni, tukamrudie Mwenyezi-Mungu! Yeye mwenyewe ameturarua, lakini yeye mwenyewe atatuponya. Yeye mwenyewe ametujeruhi, lakini yeye mwenyewe atatibu majeraha yetu.
2 Baada ya siku mbili, atatupa uhai tena, naam, siku ya tatu atatufufua ili tuweze kuishi pamoja naye.
3 Basi tumtambue, tujitahidi kumjua Mwenyezi-Mungu. Kuja kwake ni hakika kama alfajiri, yeye atatujia kama manyunyu, kama mvua za masika ziinyweshayo ardhi.’”
4 Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitakutendea nini ee Efraimu? Nikufanyie nini ee Yuda? Upendo wenu kwangu ni kama ukungu wa asubuhi, kama umande unaotoweka upesi.
5 Ndiyo maana nimewavamia kwa njia ya manabii, nimewaangamiza kwa maneno yangu, hukumu yangu huchomoza kama pambazuko.
6 Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si tambiko, Kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa. Uhalifu umeenea kote nchini
7 “Lakini mlilivunja agano langu kama mlivyofanya mjini Adamu; huko walinikosea uaminifu.
8 Gileadi ni mji wa waovu, umetapakaa damu.
9 Kama wanyang'anyi wamwoteavyo mtu njiani, ndivyo na makuhani walivyojikusanya na kuvizia. Wanaua watu njiani kuelekea Shekemu, naam, wanatenda uovu kupindukia.
10 Nimeona jambo la kuchukiza sana miongoni mwa Waisraeli: Watu wa Efraimu wanakimbilia miungu mingine naam, Waisraeli wamejitia unajisi.
11 Nawe Yuda hali kadhalika, nimekupangia wakati utakapovuna adhabu.

Generic placeholder image