14

Kumrudia Mungu na hali mpya
1 Enyi Waisraeli, mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mmejikwaa kwa sababu ya uovu wenu.
2 Ombeni toba kwake, mrudieni na kumwambia: “Utusamehe uovu wote, upokee zawadi zetu, nasi tutakusifu kwa moyo.
3 Ashuru haitatuokoa, hatutategemea tena farasi wa vita. Hatutaviita tena: ‘Mungu wetu’ hivyo vinyago tulivyochonga wenyewe. Kwako ee Mungu yatima hupata huruma.”
4 Mwenyezi-Mungu asema, “Nitaponya utovu wao wa uaminifu; nitawapenda tena kwa hiari yangu, maana sitawakasirikia tena.
5 Nitakuwa kama umande kwa Waisraeli nao watachanua kama yungiyungi, watakuwa na mizizi kama mwerezi wa Lebanoni.
6 Chipukizi zao zitatanda na kuenea, uzuri wao utakuwa kama mizeituni, harufu yao nzuri kama maua ya Lebanoni.
7 Watarudi na kuishi chini ya ulinzi wangu, watastawi kama bustani nzuri. Watachanua kama mzabibu, harufu yao nzuri kama ya divai ya Lebanoni.
8 Enyi watu wa Efraimu, mna haja gani tena na sanamu? Mimi ndiye ninayesikiliza sala zenu, mimi ndiye ninayewatunzeni. Mimi nitawapa kivuli kama mberoshi, kutoka kwangu mtapata matunda yenu.
9 Yeyote aliye na hekima ayaelewe mambo haya, mtu aliye na busara ayatambue. Maana njia za Mwenyezi-Mungu ni nyofu; watu wanyofu huzifuata, lakini wakosefu hujikwaa humo.”

Generic placeholder image