2

Mika na wapinzani wake
1 Ole wao wanaopanga kutenda maovu wanaolala usiku wakiazimia uovu! Mara tu kunapopambazuka, wanayatekeleza kwani wanao uwezo.
2 Hutamani mashamba na kuyatwaa; wakitaka nyumba, wananyakua. Huwadhulumu wenye nyumba na jamaa zao, huwanyang'anya watu mali zao.
3 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ninapanga kuwaleteeni nyinyi maafa, ambayo kamwe hamtaweza kuyakwepa. Utakuwa wakati mbaya kwenu, wala hamtaweza kwenda kwa maringo.
4 Siku hiyo watu watawasimanga kwa wimbo, watalia na kuomboleza kwa uchungu, wakisema: ‘Tumeangamia kabisa; Mwenyezi-Mungu amechukua nchi yetu, naam, ameiondoa mikononi mwetu. Mashamba yetu amewagawia waliotuteka.’”
5 Kwa hiyo hamtagawiwa sehemu yoyote ya ardhi miongoni mwa watu wake Mwenyezi-Mungu.

Wapinzani wa nabii
6 “Usituhubirie sisi. Mambo kama hayo si ya kuhubiriwa. Sisi hatutakumbwa na maafa!
7 Je, yafaa kusema hivyo, wazawa wa Yakobo? Je, Mwenyezi-Mungu ameacha uvumilivu wake? Je, yeye hufanya mambo kama haya?”

Mika
Sivyo! Maneno yangu huwafaa watendao mambo mema.
8 Lakini Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: “Nyinyi mnawavamia watu wangu kama adui. Mnawanyang'anya mavazi yao watu watulivu; watu wanaopita kwenda zao bila wasiwasi, na wasio na fikira zozote za vita.
9 Mnawafukuza wake za watu wangu kutoka nyumba zao nzuri; watoto wao mmewaondolea fahari yangu milele.
10 Inukeni mwende zenu! Hapa hamna tena pa kupumzika! Kwa utovu wenu wa uaminifu maangamizi makubwa yanawangojea!
11 Kama mtu angetokea akatamka maneno matupu ya uongo na kusema: ‘Nawatabirieni divai na pombe kwa wingi’, mhubiri wa namna hiyo angependwa na watu hawa!
12 “Lakini kweli nitawakusanya nyote enyi watu wa Yakobo, naam, nitawakusanya enyi Waisraeli mliobaki, niwalete pamoja kama kondoo katika zizi, kama kundi kubwa la kondoo malishoni; nanyi mtakuwa kundi la watu wengi.”
13 Yule atakayetoboa njia atawatangulia, nao watalivunja lango la mji na kutoka nje, watapita na kutoka nje. Mfalme wao atawatangulia; Mwenyezi-Mungu mwenyewe atawatangulia.

Generic placeholder image