6

Lalamiko la nabii
1 Sikilizeni anachosema Mwenyezi-Mungu: “Wewe nabii, nenda ukailalamikie milima, navyo vilima visikie sauti yako.”
2 Sikilizeni kesi ya Mwenyezi-Mungu enyi milima, sikilizeni enyi misingi ya kudumu ya dunia! Mwenyezi-Mungu anayo kesi dhidi ya watu wake. Yeye atatoa mashtaka dhidi ya Waisraeli.
3 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wangu, nimewatendea nini? Nimewachosha kwa kitu gani? Nijibuni!
4 Mimi niliwatoa nchini Misri; niliwakomboa kutoka utumwani; niliwapeni Mose, Aroni na Miriamu kuwaongoza.
5 Enyi watu wangu, kumbukeni njama za Balaki mfalme wa Moabu, na jinsi Balaamu mwana wa Beori alivyomjibu. Kumbukeni yaliyotukia njiani kati ya Shitimu na Gilgali. Kumbukeni mtambue matendo yangu ya kuwaokoa!”

Swali la watu
6 Nimwendee Mwenyezi-Mungu na kitu gani, nipate kumwabudu Mungu aliye juu? Je, nimwendee na sadaka za kuteketezwa, nimtolee ndama wa mwaka mmoja?
7 Je, Mwenyezi-Mungu atapendezwa nikimtolea maelfu ya kondoo madume, au mito elfu na elfu ya mafuta? Je, nimtolee mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, naam, mtoto wangu kwa ajili ya dhambi yangu?

Jibu la nabii
8 Mungu amekuonesha yaliyo mema, ewe mtu; anachotaka Mwenyezi-Mungu kwako ni hiki: Kutenda mambo ya haki, kupenda kuwa na huruma, na kuishi kwa unyenyekevu na Mungu wako.
9 Mwenyezi-Mungu anawaita wakazi wa mji, na ni jambo la busara sana kumcha yeye: “Sikilizeni, enyi watu wa Yuda; sikilizeni enyi mliokusanyika mjini.
10 “Je, nitavumilia maovu yaliyorundikwa nyumbani mwao, mali zilizopatikana kwa udanganyifu, na matumizi ya mizani danganyifu, jambo ambalo ni chukizo?
11 Je, naweza kusema hawana hatia watu wanaotumia mizani ya danganyifu na mawe ya kupimia yasiyo halali?
12 Matajiri wa miji wamejaa dhuluma, wakazi wake husema uongo, kila wasemacho ni udanganyifu.
13 Kwa hiyo nami, nimeanza kuwaangusha chini, na kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.
14 Mtakula lakini hamtashiba; ndani mwenu njaa itazidi kuwauma. Mkiweka akiba haitahifadhiwa, na mkihifadhi kitu nitakiharibu kwa vita.
15 Mtapanda mbegu, lakini hamtavuna. Mtasindika zeituni, lakini hamtatumia hayo mafuta. Mtasindika zabibu, lakini hamtakunywa hiyo divai.
16 Nyinyi mnafuata mfano mbaya wa mfalme Omri na mfano wa jamaa ya mfalme Ahabu na mfano mbaya wa jamaa ya mwanawe, Ahabu, na mmefuata mashauri yao. Kwa hiyo nitawaleteeni maangamizi, na kila mtu atawadharau. Watu watawadhihaki kila mahali.”

Generic placeholder image