5

Kiongozi mpya kutoka Bethlehemu
1 Jumuikeni mkajikusanye enyi watu wa Yerusalemu; mkisema: “Tumezingirwa, tumesongwa; naye kiongozi wa Israeli wanampiga shavuni kwa fimbo.”
2 Mwenyezi-Mungu asema, “Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha, wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda, lakini kwako kutatoka mtawala atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu. Asili yake ni ya zama za kale.”
3 Hivyo Mungu atawaacha watu wake kwa maadui, mpaka yule mama mjamzito atakapojifungua. Kisha ndugu zake waliobakia, watarudi na kuungana na Waisraeli wenzao.
4 Huyo mtawala atawachunga watu wake kwa nguvu ya Mwenyezi-Mungu, kwa fahari yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Watu wake wataishi kwa usalama, maana atakuwa mkuu mpaka miisho ya dunia.
5 Yeye ndiye atakayeleta amani.

Ukombozi na adhabu
Waashuru wakivamia nchi yetu, na kuupenya ulinzi wetu, tutapeleka walinzi wawakabili, naam, tutawapeleka viongozi wetu kwa wingi.
6 Kwa silaha zao wataitawala nchi ya Ashuru, na kuimiliki nchi ya Nimrodi. Watatuokoa mikononi mwa Waashuru, watakapowasili mipakani mwa nchi yetu na kuanza kuivamia nchi yetu.
7 Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai wameenea miongoni mwa mataifa mengi, watakuwa kama umande wa Mwenyezi-Mungu uburudishao, kama manyunyu yaangukayo penye nyasi ambayo hayasababishwi na mtu wala kumtegemea binadamu.
8 Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai, wameenea miongoni mwa mataifa na watu wengi watakuwa na nguvu kubwa kama simba kati ya wanyama wa porini, kama mwanasimba miongoni mwa makundi ya kondoo, ambaye kila mahali apitapo, huyarukia na kuyararua mawindo yake, asiwepo mtu yeyote wa kuyaokoa.
9 Waisraeli watawashinda adui zao na kuwaangamiza kabisa.
10 Mwenyezi-Mungu asema, “Wakati huo nitawaondoa farasi wenu, na kuyaharibu magari yenu ya farasi.
11 Nitaiharibu miji ya nchi yenu, na kuzibomolea mbali ngome zenu.
12 Nitatokomeza matendo yenu ya uchawi, nanyi hamtakuwa tena na wapiga ramli.
13 Nitaziharibu sanamu zenu, na nguzo zenu za ibada; nanyi mtakoma kuabudu vitu mlivyotengeneza wenyewe.
14 Nitazing'oa sanamu za Ashera kutoka kwenu, na kuiangamiza miji yenu.
15 Kwa hasira na ghadhabu yangu, nitalipiza kisasi mataifa yote yasiyonitii.”

Generic placeholder image