Des 19 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Amu.13:2–7,24–25
Siku zile, palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa
tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa,
huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai
wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume;
na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza
kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa
Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka
wapi? Wala hakuniambia jina lake; lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume;
basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa
Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake. Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake
Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahanedani,
katikati ya Sora na Eshtaoli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.71:3–6,16–17
1. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Uniamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi. (K)
(K) Kinywa changu kitajazwa sifa zako, na heshima yako mchana kutwa.
2. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. (K)
3. Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Mungu,
Nitawakumbusha watu haki yako wewe peke yako.
Ee Mungu umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee chipukizi la Yese, unayesimama kama ishara ya mataifa, usikawie kuja kutuokoa.
Aleluya.
INJILI: Lk.1:5–25
Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe
alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu,
wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti
alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya
zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana
ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika
wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto
mwanamume, na jina lake utamwita Yohane. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa
kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa roho Mtakatifu hata
tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake
katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za
wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo?
Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli,
nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu,
usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa
wakati wake. Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka
hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwashiria akakaa bubu.
Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti
alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia
ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.
------------
NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua
sehemu ya sala za waamini
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, kadiri Mkombozi anavyozidi kukaribia tunajihoji na kuona kuwa bado tunahitaji msaada wa
Mungu, ili tuweze kutimiza mapenzi yake. Na hivi tuombe: Ee Mungu Mwenyezi, twakuomba:-
Kiitikio: Sikiliza ombi letu.
1. Uzibariki juhudi za viongozi wetu wa Kanisa katika kulihubiri Neno lako na utujalie kuyafuata maonyo ya
malaika na kuzitii dhamiri zetu njema.
2. Utuepushe na ulevi, vitu najisi na anasa zote ili tudumu katika uaminifu na utii wa amri zako.
3. Utukinge na udadisi au ubishi wa bure kwa wajumbe wako watakatifu wanaotumwa kwetu.
4. Uwarehemu marehemu wetu F. na kuwapokea katika hekalu lako takatifu huko mbinguni.
Ee Mungu, Chipukizi hilo la Yese, yaani Mkombozi anayesimama kama ishara ya mataifa, asisite wala kukawia
kuja kutuokoa. Unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.