Des 20 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Isa.7:10–14
Siku zile, Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali
palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu
Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu,
hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua
mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1–6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. (K)
(K) Mfalme wa utukufu apate kuingia.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe.
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee ufunguo wa Daudi, ufunguaye milango ya ufalme wa milele, njoo kuwaokoa watu wako waliofungwa
katika gereza la giza.
Aleluya.
INJILI: Lk.1:26–38
Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali
bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni
Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika
sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope,
Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake
utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi,
baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia
malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu
yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa
kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume
katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana
kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika
akaondoka akaenda zake.
------------
NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua
sehemu ya sala za waamini
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Bwana Mungu, wewe umependa kutukomboa sisi wanadamu kwa njia ya mwanadamu; tena umekuwa mwaminifu katika
kutimiza ahadi zako. Tunapongojea kwa matumaini kuzaliwa kwa Mkombozi uliyetuahidia, twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Utujalie imani thabiti yenye kujali ishara za nyakati kwa ajili ya wokovu wetu.
2. Majina yetu ya Kikristo tuliyopewa yatukumbushe kwamba tumeahidi kukupokea na kuwa wafuasi wa Mwanao siku
zote.
3. Kwa umwilisho wa Mwanao, daima tuonje huruma na upendo wako kwetu sisi wakosefu; na tumpokee daima katika
Ekaristi Takatifu ili siku zote awe Mungu pamoja nasi.
4. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, tujaliwe upendo wa kweli, utii wa imani na utayari wa kushiriki kazi
ya ukombozi bila masharti yoyote.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.