Des 21 MAJILIO
MASOMO

SOMO 1: Sef.3:14:14–17
Imba, ee binti Sayuni; piga kelele, ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:2–3,11–12,20–21
1. Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe. (K)

(K) Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki: Mwimbieni wimbo mpya.

2. Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wako, Watu aliowachagua kuwa urithi wake. (K)

3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Maana mioyo yetu itamfurahia,
Kwa kuwa tumelitumaini jina lake takatifu. (K)

Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Utokaye Mashariki, uliye mng’ao wa mwanga wa milele na jua la haki, njoo kuwaangazia wakaao gizani na katika kivuli cha mauti.
Aleluya.

INJILI: Lk.1:39–45
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.

------------

NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua sehemu ya sala za waamini

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, ingawa Mkombozi wetu alijua kwamba angezaliwa katika mazingira ya taabu na ya kutopokeleka vizuri, alikuja kwa furaha. Basi, tumwombe katika shida zetu:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ujio wako ufungue mioyo yetu na kutuwashia mapendo kwa wote wanaotujia na kutuomba msaada.

2. Wewe unatupigia hodi kila siku ili tukupokee katika Neno lako, katika Sakramenti na katika wenzetu. Utusamehe kwa kutojua au kwa kutokujali kwetu.

3. Yohane Mbatizaji aliruka kwa shangwe tumboni mwa mamaye kuonesha furaha yake ya kukutana nawe. Utujalie nasi utimilifu wa furaha ya Noeli.

4. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama yako na mama yetu, tujaliwe upendo wa kidugu kwa wote wanaohitaji msaada wetu kama yeye alivyomtendea Elizabeti.

Ee Bwana Yesu, Mama yako aliambiwa, “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.” Basi, ututimizie hayo tunayoyangojea kwa imani na matumaini. Wewe unayeishi na kutawala na Baba na Roho Mtakatifu, Mungu daima na milele. Amina.