Des 23 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Mal.3:1-4;4:5-6
Bwana Mungu asema: angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana
mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja,
asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama
atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu
afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha
kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na
Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye
ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga
dunia kwa laana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.25:4-5,8-10,14
1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha. (K)
(K) Changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu unakaribia.
2. Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
3. Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao,
Naye atawajulisha agano lake. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Immanuel, mfalme na mwanasheria wetu, njoo ukatuokoe, ee Bwana, Mungu wetu.
Aleluya.
INJILI: Lk.1:57-66
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na
jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja
kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa
Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo
kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake
kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa
karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia
wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja
naye.
------------
NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua
sehemu ya sala za waamini
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, leo tunaambiwa Bwana ambaye ni Mjumbe wa Agano atalijia hekalu lake kwa ghafla; na tunaulizwa:
“Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake, na atakayesimama atakapoonekana yeye?” Tuombe ili
tusifadhaishwe na jambo lolote.
Kiitikio: Mungu wa huruma utusikie.
1. Kwa huruma yako ya kimungu, ututakase mioyo na roho zetu, ili tung'ae kuliko fedha na dhahabu kwa
ajili ya ujio wa Yesu Masiha wetu.
2. Wahubiri wa Neno lako wafurahie kumtambulisha kwa taifa lako Mkombozi atakayekuja, ambaye wanamhubiri
siku zote.
3. Mkombozi wetu aje aiokoe dunia yetu na laana, kwa kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na
mioyo ya watoto iwaelekee baba zao.
4. Utujalie sisi sote furaha ya Noeli pamoja na wote watakaozaliwa na Mtoto Yesu siku hiyo kimwili na
kiroho.
Ee Mwenyezi, Bwana wetu, kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, mtangulizi wa Mwanao, kulileta furaha na matumaini
makubwa kwa majirani zake Elizabeti. Utupe nasi mwamko wa kufurahia ujio wa Mkombozi wetu na kuwapokea kwa
shukrani watoto watakaozaliwa pamoja naye. Anayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.