15

Mungu ataiangamiza Moabu
1 Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Moabu. Mji wa Ari nchini Moabu umeangamizwa usiku; mji wa Kiri nchini Moabu umeteketezwa usiku.
2 Watu wa Diboni wamepanda hekaluni, hadi mahali pa juu kuomboleza, watu wa Moabu wanalia kwa ajili ya Nebo na Medeba; vichwa vyote vimenyolewa upara, ndevu zao zote zimekatwa kabisa.
3 Wanapita njiani wamevaa mavazi ya gunia. Kwenye paa za nyumba na viwanja vya mji watu wanalia na kukauka kwa machozi.
4 Watu wa Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Hata askari wa Moabu wanalia kwa sauti; mioyo yao inatetemeka.
5 Moyo wangu unasononeka juu ya nchi ya Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, wanakimbia mpaka Eglath-shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi wakilia, njiani kwenda Horonaimu wanatoa kilio cha maangamizi.
6 Kijito cha Nimrimu kimekauka; nyasi zimekauka, majani mabichi yamenyauka, hakuna chochote kinachoota hapo.
7 Watu wanavuka kijito cha Mierebi wamebeba mali yao yote waliyochuma, na kila walichojiwekea kama akiba.
8 Kilio kimezuka pote nchini Moabu, maombolezo yao yamefika Eglaimu, naam, yamefika mpaka Beer-elimu.
9 Maji ya Diboni yamejaa damu, lakini Mungu ataongeza msiba wa Diboni. Hao wachache watakaobaki hai na kukimbia kutoka nchini Moabu, watapelekewa simba wa kuwaua.

Generic placeholder image