46

1 “Wewe Beli umeanguka; Nebo umeporomoka. Wakati mmoja watu walibeba sanamu zenu. Sasa wanazibeba mgongoni mwa wanyama, hao wanyama wachovu wamelemewa.
2 Nyinyi mmeanguka na kuvunjika, hamwezi kuviokoa vinyago vyenu; nyinyi wenyewe pia mtapelekwa uhamishoni!
3 “Sikilizeni enyi wazawa wa Yakobo, nisikilizeni enyi mabaki ya watu wangu wa Israeli. Mimi niliwatunzeni tangu mlipozaliwa; niliwabebeni tangu tumboni mwa mama yenu.
4 Mimi ni yuleyule hata katika uzee wenu; hata katika uzee wenu mimi nitawabeba. Nilifanya hivyo kwanza, nitafanya hivyo tena. Nitawabeba nyinyi na kuwaokoa.
5 “Mtanifananisha na nani, tufanane? Je, mwaweza kunilinganisha na nani, tulingane?
6 Watu humimina dhahabu kutoka mifuko yao, hupima fedha kwenye mizani zao, wakamwajiri mfua dhahabu atengeneze sanamu kisha huisujudu na kuiabudu!
7 Hujitwisha sanamu hiyo mabegani, wakaibeba, kisha huiweka mahali pake, ikakaa papo hapo; kamwe haiwezi hata kusogea kutoka hapo ilipo. Mtu akiililia, haiwezi kumwitikia, wala haiwezi kumwokoa mtu katika taabu zake.
8 “Kumbukeni jambo hili na kutafakari, liwazeni akilini mwenu enyi wakosefu.
9 Kumbukeni mambo niliyotenda hapo kale! Mimi ndimi Mungu na hakuna mwingine; naam, mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine kama mimi.
10 Nilitangaza mambo ya mwisho tangu mwanzo, tangu kale nilitangaza mambo yatakayotukia. Lengo langu litatimia; mimi nitatekeleza nia yangu yote.
11 Ninamwita tai wangu kutoka mashariki, naam, msiri wangu kutoka nchi ya mbali. Mimi nimenena na nitayafanya; mimi nimepanga nami nitatekeleza.
12 “Nisikilizeni, enyi wenye vichwa vigumu, nisikilizeni enyi mlio mbali na ukombozi.
13 Siku ya kuwakomboa naileta karibu, haiko mbali tena; siku ya kuwaokoeni haitachelewa. Nitauokoa mji wa Siyoni, kwa ajili ya Israeli, fahari yangu.

Generic placeholder image