52
Mungu ataikomboa Yerusalemu 1 Amka! Amka! Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni! Jivike mavazi yako mazuri, ewe Yerusalemu, mji mtakatifu. Maana hawataingia tena kwako watu wasiotahiriwa na walio najisi. 2 Jikungute mavumbi, uinuke ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara! Jifungue minyororo yako shingoni, ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka. 3 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja. 4 Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote. 5 Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku. 6 Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!” 7 Tazama inavyopendeza kumwona mjumbe akitokea mlimani, ambaye anatangaza amani, ambaye analeta habari njema, na kutangaza ukombozi! Anauambia mji wa Siyoni: “Mungu wako anatawala!” 8 Sikiliza sauti ya walinzi wako; wanaimba pamoja kwa furaha, maana wanaona kwa macho yao wenyewe, kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni. 9 Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu! Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, ameukomboa mji wa Yerusalemu. 10 Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu, mbele ya mataifa yote. Atawaokoa watu wake, na ulimwengu wote utashuhudia. 11 Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa; msiguse kitu chochote najisi! Ondokeni huku Babuloni! Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu. 12 Safari hii hamtatoka kwa haraka, wala hamtaondoka mbiombio! Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni, Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma. Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu 13 Mungu asema hivi: “Mtumishi wangu atafanikiwa; atatukuzwa na kupewa cheo, atapata heshima kuu. 14 Wengi waliomwona walishtuka, kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa; hakuwa tena na umbo la kibinadamu! 15 Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi. Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake, maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa, na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”