31

Misri haitaweza kusaidia
1 Ole wao wale waendao Misri kuomba msaada, ole wao wanaotegemea farasi, wanaotegemea wingi wa magari yao ya vita, na nguvu za askari wao wapandafarasi, nao hawamtegemei Mtakatifu wa Israeli, wala hawamwombi Mwenyezi-Mungu shauri!
2 Mungu ni mwenye busara na huleta maangamizi. Habadilishi tamko lake; ila yuko tayari kuwakabili watu waovu kadhalika na wasaidizi wa watendao mabaya.
3 Wamisri ni binadamu tu wala si Mungu; farasi wao nao ni wanyama tu, si roho. Mwenyezi-Mungu akiunyosha mkono wake, taifa linalotoa msaada litajikwaa, na lile linalosaidiwa litaanguka; yote mawili yataangamia pamoja.

Mungu ataulinda mji wa Yerusalemu
4 Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Kama vile simba au mwanasimba angurumavyo kuyakinga mawindo yake, hata kundi la wachungaji likiitwa kumkabili, yeye hatishiki kwa kelele zao, wala hashtuki kwa sauti zao. Ndivyo atakavyoshuka Mwenyezi-Mungu wa majeshi kupigana juu ya mlima Siyoni na kilima chake.
5 Kama ndege arukavyo juu ya viota vyake, ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyoulinda Yerusalemu, ataulinda na kuukomboa, atauhifadhi na kuuokoa.
6 Enyi Waisraeli, mrudieni huyo mliyemsaliti vibaya.
7 Wakati utafika ambapo nyote mtavitupilia mbali vinyago vyenu vya fedha na dhahabu ambavyo mmejitengenezea kwa mikono yenu, vikawakosesha.
8 Hapo Waashuru watauawa kwa upanga, lakini si kwa upanga wa binadamu; naam, wataangamizwa kwa upanga ambao ni zaidi ya ule wa binadamu. Waashuru watakimbia na vijana wao watafanyizwa kazi za kitumwa.
9 Mfalme wao atatoroka kwa hofu, na maofisa wao wataiacha bendera yao kwa woga. Hayo ameyatamka Mwenyezi-Mungu ambaye moto wake umo mjini Siyoni, naam, tanuri lake limo mjini Yerusalemu.”

Generic placeholder image