17

Maji kutoka mwambani
(Hes 20:1-13)
1 Kutoka jangwa la Sini, jumuiya yote ya Waisraeli ilisafiri hatua kwa hatua kama alivyoamuru Mwenyezi-Mungu, watu wakapiga kambi huko Refidimu. Lakini huko hakukuwa na maji ya kunywa.
2 Kwa hiyo watu wakamnungunikia Musa wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Musa akawauliza, “Mbona mnaninungunikia? Mbona mnamjaribu Mwenyezi-Mungu?”
3 Lakini wote walikuwa na kiu, wakamnungunikia Musa wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri utuue kwa kiu sisi sote na watoto wetu na mifugo yetu?”
4 Basi, Musa akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nitawafanyia nini watu hawa? Wako karibu kunipiga mawe!”
5 Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Pita mbele ya watu hawa ukiwachukua wazee wao kadhaa; chukua pia mkononi mwako ile fimbo uliyoipiga nayo mto Nili.
6 Tazama mimi nitasimama mbele yako mwambani pale Horebu, nawe utaupiga huo mwamba na maji yatabubujika kutoka humo ili watu wote wapate kunywa.” Basi, Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Waisraeli.
7 Mahali hapo Musa akapaita “Masa” na “Meriba”, kwa sababu Waisraeli walimnungunikia na kumjaribu Mwenyezi-Mungu wakisema, “Je, kweli Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi?”

Vita na Waamaleki
8 Waamaleki walikuja na kupigana na Waisraeli huko Refidimu.
9 Musa akamwambia Yoshua, “Chagua wanaume uende ukapigane na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilele cha kilima, nikiishika mkononi mwangu ile fimbo ya Mungu.”
10 Basi, Yoshua akafanya kama Musa alivyosema, akaenda kupigana na Waamaleki. Musa, Aroni na Huri wakapanda kilele cha kilima.
11 Ikawa wakati wote Musa alipoinua mkono wake juu, Waisraeli walishinda, na alipouteremsha, Waamaleki walishinda.
12 Lakini baada ya muda, mikono ya Musa ilichoka. Kwa hiyo Aroni na Huri walichukua jiwe wakaliweka karibu na Musa naye akaketi. Kisha wakaishika na kuiinua mikono yake, mmoja akauinua mkono wa kulia na mwingine mkono wa kushoto. Hivyo mikono ya Musa ikabaki imara ikiwa imeinuliwa juu hadi jua lilipotua.
13 Yoshua akawakatakata Waamaleki.
14 Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Liandike jambo hili katika kitabu, liwe ukumbusho. Tena kariri masikioni mwa Yoshua kwamba nitawafuta kabisa Waamaleki duniani.”
15 Musa akajenga madhabahu na kuiita, “Mwenyezi-Mungu ni Bendera Yangu”,
16 akisema, “Inueni juu bendera ya Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu atapigana na Waamaleki kizazi hata kizazi!”

Generic placeholder image