5
Musa na Aroni mbele ya Farao
1 Baadaye, Musa na Aroni walimwendea Farao, wakamwambia, âMwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli anasema hivi, âWaache watu wangu waondoke, wakanifanyie sikukuu jangwani.ââ
2 Lakini Farao akawauliza, âNi nani huyo Mwenyezi-Mungu, hata nimsikilize na kuwaacha Waisraeli waondoke? Mimi simtambui huyo Mwenyezi-Mungu, wala sitawaruhusu Waisraeli waondoke.â
3 Musa na Aroni wakamwambia, âMungu wa Waebrania amekutana nasi. Tunakusihi utuache twende zetu jangwani mwendo wa siku tatu tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. La sivyo, yeye atatuua kwa maradhi mabaya au vita.â
4 Lakini mfalme wa Misri akawajibu, âEnyi Musa na Aroni, kwa nini mnajaribu kuwatoa watu kazini mwao? Rudini kazini mwenu.â
5 Tena Farao akasema, âHawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!â
6 Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema,
7 âTangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia.
8 Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: âTuache twende tukamtambikie Mungu wetu.â
9 Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.â
10 Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, âFarao anasema hivi, âSitawapeni nyasi.
11 Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.ââ
12 Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali.
13 Nao Wanyapara wakakazana wakisema, âTimizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.â
14 Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, âKwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?â
15 Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, âKwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako?
16 Hatupewi tena nyasi zozote na huku tunalazimishwa kufyatua matofali. Tena sisi watumishi wako tunapigwa, hali kosa ni la watu wako.â
17 Lakini Farao akasema, âWavivu nyinyi; nyinyi ni wavivu, ndio maana mnasema, âTuache twende tukamtambikie Mwenyezi-Munguâ.
18 Nendeni sasa mkafanye kazi; maana hamtapewa nyasi zozote na mtafyatua idadi ileile ya matofali.â
19 Basi, hao wasimamizi wa Waisraeli sasa walijiona kuwa wako taabuni, kwani waliambiwa, âHamtaipunguza kamwe idadi ya matofali ya kila siku.â
20 Walipoondoka kwa Farao, walikutana na Musa na Aroni ambao walikuwa wanawangojea.
21 Basi, wakawaambia Musa na Aroni, âMwenyezi-Mungu na aone jambo hili na kuwahukumu nyinyi kwa sababu mmetufanya sisi kuwa chukizo kwa Farao na maofisa wake; nyinyi mmewapa sababu ya kutuua.â
Musa anamlalamikia Mwenyezi-Mungu
22 Kisha Musa akamgeukia tena Mwenyezi-Mungu, akasema, âEe Mwenyezi-Mungu, kwa nini unawatendea watu hawa uovu? Kwa nini hata ulinituma?
23 Tangu nilipokwenda na kuongea na Farao kwa jina lako, yeye amewatendea uovu watu hawa. Wewe hujafanya lolote kuwakomboa watu wako.â