4

Musa apewa uwezo wa kufanya miujiza
1 Musa akamwambia Mungu, “Lakini Waisraeli hawataniamini wala kunisikiliza, bali watasema kuwa wewe Mwenyezi-Mungu hukunitokea.”
2 Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Unashika nini mkononi mwako?” Musa akamwambia, “Fimbo.”
3 Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Itupe chini.” Musa akaitupa fimbo chini, nayo ikageuka kuwa nyoka! Musa akaikimbia.
4 Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Nyosha mkono wako, umkamate mkia!” Musa akanyosha mkono wake, akamkamata; nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake.
5 Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Hivyo Waisraeli watapata kuamini kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, nimekutokea.”
6 Tena, Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Ingiza mkono wako kifuani mwako.” Musa akafanya hivyo, lakini alipoutoa nje, kumbe ukawa na ukoma; mweupe kama theluji.
7 Kisha Mungu akamwambia, “Ingiza tena mkono wako kifuani mwako!” Musa akauingiza mkono wake kifuani. Na alipoutoa nje, kumbe ukarudia hali yake ya kawaida kama ulivyo mwili wake.
8 Mungu akamwambia Musa, “Wasipokuamini au kusadiki ishara ya kwanza, yawezekana wakaamini ishara ya pili.
9 Lakini wasipoamini hata ishara hizi mbili, au kuamini maneno yako, utachota maji ya mto Nili na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Maji hayo yatakuwa damu juu ya nchi kavu.”
10 Lakini Musa akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Ewe Bwana wangu, mimi sina ufasaha wa kuongea tangu zamani; hata baada ya wewe kusema nami mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito.”
11 Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Ni nani aliyeumba kinywa cha mtu? Ni nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi? Aone au awe kipofu? Je, si mimi Mwenyezi-Mungu?
12 Basi, nenda! Mimi nitakiongoza kinywa chako na kukufundisha cha kusema.”
13 Lakini Musa akasema, “Ee Bwana wangu, tafadhali nakusihi, umtume mtu mwingine.”
14 Ndipo hasira ya Mungu ilipowaka dhidi ya Musa, akamwambia, “Je, si yuko ndugu yako Aroni ambaye ni Mlawi? Najua yeye ana ufasaha wa kuongea. Tena anakuja kukutana nawe, na mara tu atakapokuona atafurahi moyoni.
15 Wewe utaongea naye na kumwambia yote atakayosema. Mimi nitawasaidieni na kuwafundisha mambo mtakayofanya.
16 Aroni ataongea na Waisraeli kwa niaba yako. Yeye atakuwa msemaji wako, nawe utakuwa kama Mungu kwake.
17 Utaichukua mkononi mwako fimbo hii ambayo utaitumia kufanya zile ishara.”

Musa anarudi Misri
18 Musa alirudi kwa Yethro, baba mkwe wake, akamwambia, “Tafadhali niruhusu nirudi Misri kwa ndugu zangu, nikaone kama bado wako hai.” Yethro akamwambia, “Nenda kwa amani.”
19 Musa akiwa bado nchini Midiani, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi Misri kwa sababu wale wote waliotaka kukuua wamekwisha kufa.”
20 Basi, Musa akamchukua mkewe na watoto wake, akawapandisha juu ya punda, akaanza safari ya kurudi Misri. Mkononi mwake alichukua ile fimbo aliyoamriwa na Mungu aichukue.
21 Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Utakapofika Misri, hakikisha kwamba umetenda mbele ya Farao miujiza yote niliyokupa uwezo kuifanya. Lakini mimi nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hatawaachia Waisraeli waondoke.
22 Nawe utamwambia Farao kuwa Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume!
23 Nami nakuambia: Mwache mwanangu aondoke, ili anitumikie! Kama ukikataa kumwachia aondoke, tazama nitamuua mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.’”
24 Akiwa bado njiani kurudi Misri, Musa alikuwa mahali pa kulala wageni; basi, Mungu alikutana naye na kutaka kumuua.
25 Hapo Zipora akakimbia haraka, akachukua jiwe kali, akalikata govi la mwanawe na kumgusa nalo Musa miguuni akisema, “Wewe ni bwana harusi wa damu”.
26 Hapo Mwenyezi-Mungu akamwacha Musa. Zipora alikuwa amesema, “Bwana harusi wa damu,” kwa sababu ya kutahiri.
27 Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukakutane na Musa.” Basi, Aroni akaenda, akakutana na Musa kwenye mlima wa Mungu, akambusu.
28 Naye Musa akamwambia Aroni maneno yote aliyoambiwa na Mwenyezi-Mungu ayaseme, na miujiza yote aliyoagizwa atende.
29 Kisha Musa na Aroni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli.
30 Aroni akawaambia maneno yote Mwenyezi-Mungu aliyokuwa amemwagiza Musa, na kuifanya ile miujiza mbele ya watu wote.
31 Watu wakaamini. Na waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu amewajia kuwasaidia Waisraeli, na kwamba ameyaona mateso yao, wote wakainamisha vichwa vyao na kumwabudu.

Generic placeholder image