2

Mtoto Musa anaokotwa mtoni Nili
1 Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa Walawi aliyemwoa mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa wa ukoo wa Walawi.
2 Basi, mama huyu akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Alipoona kwamba mtoto huyo mchanga alikuwa mzuri, akamficha kwa muda wa miezi mitatu.
3 Lakini kwa vile hakuweza kumficha zaidi ya muda huo, alitengeneza namna ya kikapu cha mafunjo, akakipaka namna ya lami, akamtia huyo mtoto ndani. Kisha akakiweka kikapu kando ya mto Nili kwenye majani.
4 Dada yake huyo mtoto akajificha karibu na mahali hapo ili aone yatakayompata nduguye.
5 Basi, binti Farao akashuka mtoni kuoga, na watumishi wake wakawa wanatembeatembea kandokando ya mto. Binti Farao akakiona kile kikapu katika majani, akamtuma mjakazi wake akichukue.
6 Alipokifungua, alimwona yule mtoto mchanga, analia. Basi, akamwonea huruma, akasema, “Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.”
7 Papo hapo dada yake yule mtoto akajitokeza, akamwambia binti Farao, “Je, niende nikakutafutie yaya miongoni mwa wanawake wa Kiebrania akulelee mtoto huyu?”
8 Binti Farao akamwambia, “Naam; nenda.” Basi, huyo msichana akaenda, akamwita mama yake huyo mtoto.
9 Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea.
10 Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Musa.

Musa anakimbilia Midiani
11 Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Musa.
12 Musa akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani.
13 Kesho yake, Musa alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?”
14 Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Musa aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!”
15 Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Musa. Lakini Musa alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani. Siku moja, Musa alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji.
16 Basi, binti saba wa kuhani mmoja wa huko Midiani walifika kuchota maji na kuwanywesha kondoo na mbuzi wa baba yao.
17 Wachungaji wengine wakaja na kuwafukuza hao binti. Lakini Musa akawasaidia binti hao na kuwanywesha wanyama wao.
18 Walipomrudia baba yao Reueli, yeye akawauliza, “Mbona leo mmerudi upesi hivyo?”
19 Nao wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa mikononi mwa wale wachungaji, naye mwenyewe akachota maji na kuwanywesha wanyama wetu.”
20 Baba yao akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwiteni aje ale chakula.”
21 Musa akakubali kukaa kwa huyo mtu. Basi, huyo mtu akampa Musa binti yake aitwaye Zipora awe mke wake.
22 Zipora akamzalia mtoto wa kiume. Musa akasema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni”, kwa hiyo akampa huyo mtoto jina Gershomu.

Kilio cha Waisraeli utumwani
23 Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakapiga kite na kulia kutokana na hali yao ya utumwa, na kilio chao kikamfikia Mungu juu.
24 Mungu akasikia kilio chao, naye akakumbuka agano alilofanya na Abrahamu, na Isaka na Yakobo.
25 Mungu aliwaangalia Waisraeli, akaona kuwa hali yao ni mbaya.

Generic placeholder image