16
Jibu la Ayubu 1 Hapo Ayubu akajibu: 2 “Mambo kama hayo nimeyasikia mengi; nyinyi ni wafariji duni kabisa! 3 Mwisho wa maneno haya matupu ni lini? Au ni kitu gani kinachowachochea kujibu? 4 Kama nyinyi mngekuwa mimi, na mimi nyinyi, ningeweza kusema kama nyinyi ningeweza kubuni maneno dhidi yenu, na kutikisa kichwa changu. 5 Ningeweza kuwatia moyo kwa maneno yangu, na maneno yangu ya faraja yangewatuliza. 6 “Lakini nikisema maumivu yangu hayatulii, na nikikaa kimya hayaondoki. 7 Kweli Mungu amenichakaza ameharibu kila kitu karibu nami. 8 Amenifanya ninyauke, na huo ni ushindi dhidi yangu. Kukonda kwangu kumenikabili na kushuhudia dhidi yangu. 9 Amenirarua kwa hasira na kunichukia; amenisagia meno; na adui yangu ananikodolea macho. 10 Watu wananidhihaki na kunicheka; makundi kwa makundi hunizunguka, na kunipiga makofi mashavuni. 11 Mungu amenitia mikononi mwa wajeuri, na kunitupa mikononi mwa waovu. 12 Nilikuwa nimestarehe, lakini akanivunjavunja, alinikaba shingo na kunipasua vipandevipande; alinifanya shabaha ya mishale yake, 13 akanipiga mishale kutoka kila upande. Amenipasua figo bila huruma, na nyongo yangu akaimwaga chini. 14 Hunivunja na kunipiga tena na tena; hunishambulia kama askari. 15 “Nimejishonea mavazi ya gunia, fahari yangu nimeibwaga mavumbini. 16 Uso wangu ni mwekundu kwa kulia, kope zangu zimekuwa nyeusi ti; 17 ingawa sijafanya dhuluma kwa mkono wangu, na sala zangu kwa Mungu ni safi. 18 “Ewe dunia, usiifunike damu yangu iliyomwagika; kilio changu kienee kila mahali. 19 Nina hakika ninaye shahidi wangu mbinguni, mwenye kunitetea yuko huko juu. 20 Rafiki zangu wanidharau; nabubujika machozi kumwomba Mungu. 21 Laiti mtu angenitetea mbele ya Mungu, kama ifanyikavyo duniani kati za watu wawili. 22 Naam, miaka yangu ni michache, nami nitakwenda huko ambako sitarudi.