2

Jaribio la pili
1 Ikatokea tena siku nyingine, malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani akajitokeza pia pamoja nao.
2 Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.”
3 Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Ayubu? Duniani hakuna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu. Yeye yuko imara katika unyofu wake, ingawa wewe umenichochea nimwangamize bure.”
4 Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mtu hutoa kila kitu alicho nacho ili aokoe uhai wake.
5 Lakini sasa hebu nyosha mkono wako umguse mwili wake; nakuambia atakutukana waziwazi.”
6 Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya! Waweza kumfanya utakavyo, walakini usimuue.”
7 Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamtesa Ayubu kwa madonda mabaya tangu wayo wa mguu wake mpaka utosini mwake.
8 Ayubu akatwaa kigae, akajikuna nacho na kuketi kwenye majivu.
9 Mkewe akamwambia, “Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe.”
10 Ayubu akamjibu mkewe, “Wewe unaongea kama wanawake wapumbavu. Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kupokea pia mabaya kutoka kwake?” Katika mambo hayo yote, Ayubu hakutamka neno lolote la kumkosea Mungu.

Marafiki watatu wa Ayubu wawasili
11 Marafiki watatu wa Ayubu: Elifazi kutoka Temani, Bildadi kutoka Shua na Sofari kutoka Naamathi, walisikia juu ya maafa yote yaliyompata Ayubu. Basi, wakaamua kwa pamoja waende kumpa pole na kumfariji.
12 Walipomwona kwa mbali hawakumtambua. Basi, wakaanza kupaza sauti na kulia; waliyararua mavazi yao, wakarusha mavumbi angani na juu ya vichwa vyao.
13 Kisha wakaketi udongoni pamoja na Ayubu kwa siku saba, mchana na usiku, bila kumwambia neno lolote kwani waliyaona mateso yake kuwa makubwa mno.

Generic placeholder image