30

1 “Lakini sasa watu wananidhihaki, tena watu walio wadogo kuliko mimi; watu ambao baba zao niliwaona hawafai hata kuwaangalia mbwa wangu wakilinda kondoo.
2 Ningepata faida gani mikononi mwao, watu ambao nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3 Katika ufukara na njaa kali walitafutatafuta cha kutafuna nyikani sehemu tupu zisizokuwa na chakula.
4 Walichuma mimea jangwani na majani msituni wakala, walikula hata mizizi ya mti wa mfagio.
5 Walifukuzwa mbali na watu, watu waliwapigia kelele kama wezi.
6 Iliwapasa kutafuta usalama mapangoni, kwenye mashimo ardhini na miambani.
7 Huko vichakani walilia kama wanyama, walikusanyika pamoja chini ya upupu.
8 Walikuwa wapumbavu wakuu na mabaradhuli ambao walilazimika kufukuzwa nchini kwa kiboko.
9 “Na sasa wamenitungia wimbo wa kunizomea, nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10 Wananichukia na kuniepa; wakiniona tu wanatema mate.
11 Kwa kuwa Mungu amenidhoofisha na kuniaibisha, wamekuwa huru kunitendea wapendavyo.
12 Genge la watu lainuka kunishtaki likitafuta kuniangusha kwa kunitegea. Linanishambulia ili niangamie.
13 Watu hao hukata njia yangu huchochea balaa yangu, na hapana mtu wa kuwazuia.
14 Wanakuja kama kwenye ufa mkubwa, na baada ya shambulio wanasonga mbele.
15 Hofu kuu imenishika; hadhi yangu imetoweka kama kwa upepo, na ufanisi wangu umepita kama wingu.
16 “Sasa sina nguvu yoyote nafsini mwangu; siku za mateso zimenikumba.
17 Usiku mifupa yangu yote huuma, maumivu yanayonitafuna hayapoi.
18 Mungu amenikaba kwa mavazi yangu, amenibana kama ukosi wa shati langu.
19 Amenibwaga matopeni; nimekuwa kama majivu na mavumbi.
20 Nakulilia, lakini hunijibu, nasimama kuomba lakini hunisikilizi.
21 Umegeuka kuwa mkatili kwangu, wanitesa kwa mkono wako wenye nguvu.
22 Wanitupa katika upepo na kunipeperusha; wanisukasuka huku na huko katika dhoruba kali.
23 Naam! Najua utanipeleka tu kifoni, mahali watakapokutana wote waishio.
24 “Je, mtu akikumbwa na maangamizi hainui mkono? Je, mtu akiwa taabuni haombi msaada
25 Je, sikuwalilia wale waliokuwa na taabu? Je, sikuona uchungu kwa ajili ya maskini?
26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinipata, nilipongojea mwanga, giza lilikuja.
27 Moyo wangu wahangaika wala hautulii kamwe; siku za mateso zimekumbana nami.
28 Napitapita nikiomboleza, kwangu hamna jua. Nasimama hadharani kuomba msaada.
29 Kwa kilio nimekuwa ndugu yake mbwamwitu, mimi na mbuni hamna tofauti.
30 Ngozi yangu imebambuka mifupa yangu inaungua kwa homa.
31 Kinubi changu kimekuwa cha kufanya matanga filimbi yangu kwa ajili ya kuomboleza.

Generic placeholder image