42

1 Kisha Ayubu akamjibu Mwenyezi-Mungu:
2 “Najua kwamba waweza kila kitu, lolote unalokusudia haliwezi kuzuiliwa.
3 Ulisema kuwa nilithubutu kutatiza mpango wako kijinga. Kweli nilitamka kitu ambacho sikuelewa mambo ya ajabu mno kwangu ambayo sikuwa ninayajua.
4 Uliniambia nisikilize nawe utaniambia; kwamba utaniuliza nami nikujibu.
5 Kweli nilikuwa nimesikia habari zako kwa masikio tu, lakini sasa nakuona kwa macho yangu mwenyewe.
6 Kwa hiyo natubu pamoja na kujipaka mavumbi na majivu, najiona mimi mwenyewe kuwa si kitu kabisa.”

Hatima
7 Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Ayubu, alimwambia Elifazi, Mtemani, “Ghadhabu yangu imewaka dhidi yako na marafiki zako wawili kwani hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Ayubu alivyofanya.
8 Kwa hiyo chukueni mafahali saba na kondoo madume saba, mwende kwa mtumishi wangu Ayubu, mkawatoe sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yenu. Naye mtumishi wangu Ayubu atawaombeeni, nami nitaisikiliza sala yake na kuacha kuwatenda kulingana na upumbavu wenu; maana hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Ayubu alivyofanya.”
9 Basi, Elifazi Mtemani, Bildadi, Mshua na Sofari Mnaamathi, wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaambia. Mwenyezi-Mungu akaipokea sala ya Ayubu.
10 Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi-Mungu akamrudishia Ayubu hali yake ya kwanza. Alimpa maradufu ya yote aliyokuwa nayo hapo awali.
11 Kisha ndugu zake, dada zake na rafiki wote waliomfahamu hapo awali wakamwendea nyumbani kwake, wakala chakula pamoja naye. Wakampa pole na kumfariji kwa ajili ya mateso yote ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemletea. Kila mmoja wao akampa Ayubu fedha na pete ya dhahabu.
12 Katika miaka ya Ayubu iliyofuata Mwenyezi-Mungu alimbariki zaidi kuliko hata alivyokuwa amembariki pale awali. Basi Ayubu akawa na kondoo 14,000, ngamia 6,000, ng'ombe 2,000 na punda majike 1,000.
13 Alikuwa pia na watoto wa kiume saba na wa kike watatu.
14 Binti yake wa kwanza alimpa jina Yemima, wa pili Kezia, na wa mwisho Keren-hapuki.
15 Katika nchi yote hiyo hapakuwa na wanawake waliokuwa wazuri kama mabinti wa Ayubu. Baba yao akawaachia urithi kama alivyowaachia kaka zao.
16 Baada ya hapo, Ayubu aliishi miaka 140, akawaona wajukuu na vitukuu vyake vyote hadi kizazi cha nne.
17 Basi, Ayubu akafariki akiwa mzee wa miaka mingi.

Generic placeholder image