KITABU CHA KWANZA
(Zaburi 1–41)

1

Furaha ya kweli
1 Heri mtu asiyefuata shauri la waovu, asiyeshiriki njia za wenye dhambi, wala kujumuika na wenye dharau;
2 bali huifurahia sheria ya Mwenyezi-Mungu, na kuitafakari mchana na usiku.
3 Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito, unaozaa matunda kwa wakati wake, na majani yake hayanyauki. Kila afanyalo hufanikiwa.
4 Lakini waovu sivyo walivyo; wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5 Kwa hiyo watu waovu wataanguka wakati wa hukumu, wenye dhambi hawatakaa na kusanyiko la waadilifu.
6 Maana Mwenyezi-Mungu huziongoza njia za waadilifu; lakini njia za waovu zitaishia katika maangamizi.

Generic placeholder image