149

Wimbo wa ushindi
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya; msifuni katika kusanyiko la waaminifu!
2 Furahi ee Israeli kwa sababu ya Muumba wako, wakazi wa Siyoni shangilieni kwa sababu ya Mfalme wenu.
3 Lisifuni jina lake kwa ngoma, mwimbieni kwa ngoma na zeze.
4 Maana Mwenyezi-Mungu hupendezwa na watu wake; yeye huwapamba wanyonge kwa ushindi.
5 Watu waaminifu wafurahi kwa fahari; washangilie hata walalapo.
6 Wabubujike sifa kuu za Mungu, na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
7 wawalipe kisasi watu wa mataifa, wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo, na viongozi wao kwa pingu za chuma,
9 kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa! Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu. Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image