108

Sala ya kujikinga na maadui
(Zaburi ya Daudi: Wimbo)
1 Niko thabiti moyoni, ee Mungu, naam, niko thabiti moyoni; nitaimba na kukushangilia! Amka, ee nafsi yangu!
2 Amkeni enyi kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko!
3 Ee Mwenyezi-Mungu, nitakushukuru kati ya mataifa; nitakuimbia sifa kati ya mataifa.
4 Fadhili zako ni kubwa kuliko mbingu; uaminifu wako waenea hata mawinguni.
5 Utukuzwe, ee Mungu juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote!
6 Watu hao uwapendao na wasalimishwe; utusaidie kwa mkono wako na kutusikiliza.
7 Mungu amesema kutoka patakatifu pake: “Sasa nitaigawa Shekemu kwa shangwe, bonde la Sukothi nitalipima sehemusehemu.
8 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni kofia yangu ya chuma, na Yuda ni fimbo yangu ya enzi.
9 Moabu ni kama bakuli langu la kunawia; kiatu changu nitaitupia Edomu kuimiliki. Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia!”
10 Ni nani, atakayenipeleka kwenye mji wa ngome? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?
11 Je, umetuacha kabisa, ee Mungu? Wewe huendi tena na majeshi yetu!
12 Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu, maana msaada wa binadamu haufai kitu.
13 Mungu akiwa upande wetu tutashinda, yeye atawaponda maadui zetu.

Generic placeholder image