14

Uovu wa watu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Wapumbavu hujisemea moyoni: “Hakuna Mungu.” Wote wamepotoka kabisa, wametenda mambo ya kuchukiza; hakuna hata mmoja atendaye jema!
2 Mwenyezi-Mungu anawaangalia wanadamu kutoka mbinguni, aone kama kuna yeyote mwenye busara, kama kuna yeyote anayemtafuta Mungu.
3 Lakini wote wamekosa, wote wamepotoka pamoja; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.
4 “Je, hao watendao maovu hawana akili? Wanawatafuna watu wangu kama mikate; wala hawanijali mimi Mwenyezi-Mungu.”
5 Hapo watashikwa na hofu kubwa, maana Mungu yu pamoja na waadilifu.
6 Unaweza kuvuruga mipango ya maskini, lakini Mwenyezi-Mungu ndiye kimbilio lake.
7 Laiti ukombozi wa Israeli ungefika kutoka Siyoni! Mwenyezi-Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake, wazawa wa Yakobo watashangilia; Waisraeli watafurahi.

Generic placeholder image