116

Shukrani kwa kuokolewa kifoni
1 Nampenda Mwenyezi-Mungu, kwa maana anisikia, maana amesikia kilio cha ombi langu.
2 Yeye amenitegea sikio, hivyo nitamwomba muda wote niishio.
3 Hatari ya kifo ilinizunguka, vitisho vya kaburi vilinivamia; nilijawa na mahangaiko na majonzi.
4 Kisha nikamlilia Mwenyezi-Mungu: “Ee Mwenyezi-Mungu, tafadhali unisalimishe!”
5 Mwenyezi-Mungu amejaa wema na uaminifu; Mungu wetu ni mwenye huruma.
6 Mwenyezi-Mungu huwalinda wanyofu; nilipokuwa nimekandamizwa aliniokoa.
7 Uwe na utulivu mkuu, ee nafsi yangu, maana Mwenyezi-Mungu amenitendea mema.
8 Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu; akanilinda nisije nikaanguka.
9 Nitatembea mbele yake Mwenyezi-Mungu, katika nchi ya watu walio hai.
10 Nilikuwa na imani hata niliposema: “Mimi nimetaabika mno.”
11 Hata nilisema kwa hofu yangu: “Binadamu wote hawaaminiki!”
12 Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu wote alionitendea?
13 Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa, nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu.
14 Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu, mbele ya watu wake wote.
15 Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu si jambo dogo mbele yake.
16 Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako; ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako; umenifungulia vifungo vyangu.
17 Nitakutolea tambiko za shukrani, na kukupa heshima zangu.
18 Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu mbele ya watu wako wote,
19 waliokusanyika hekaluni mwako, katikati ya Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image