97

Mungu mtawala mkuu
1 Mwenyezi-Mungu anatawala! Furahi, ee dunia! Furahini enyi visiwa vingi!
2 Mawingu na giza nene vyamzunguka; uadilifu na haki ni msingi wa utawala wake.
3 Moto watangulia mbele yake, na kuwateketeza maadui zake pande zote.
4 Umeme wake wauangaza ulimwengu; dunia yauona na kutetemeka.
5 Milima yayeyuka kama nta mbele ya Mwenyezi-Mungu; naam, mbele ya Bwana wa dunia yote.
6 Mbingu zatangaza uadilifu wake; na mataifa yote yauona utukufu wake.
7 Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa, naam, wote wanaojisifia miungu duni; miungu yote husujudu mbele zake.
8 Watu wa Siyoni wanafurahi; watu wa Yuda wanashangilia, kwa sababu ya hukumu zako, ee Mungu.
9 Wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu juu ya dunia yote; wewe watukuka juu ya miungu yote.
10 Mwenyezi-Mungu huwapenda wanaochukia uovu, huyalinda maisha ya watu wake; huwaokoa makuchani mwa waovu.
11 Mwanga humwangazia mtu mwadilifu, na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
12 Furahini kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu; mshukuruni kwa ajili ya jina lake takatifu.

Generic placeholder image