92

Wimbo wa kumsifu Mungu
(Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato)
1 Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu.
2 Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu wako nyakati za usiku,
3 kwa muziki wa zeze na kinubi, kwa sauti tamu ya zeze.
4 Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.
5 Matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, ni makuu mno! Mawazo yako ni mazito mno!
6 Mtu mpumbavu hawezi kufahamu, wala mjinga hajui jambo hili:
7 Kwamba waovu waweza kustawi kama nyasi, watenda maovu wote waweza kufanikiwa, lakini mwisho wao ni kuangamia milele,
8 bali wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u mkuu milele.
9 Hao maadui zako, ee Mwenyezi-Mungu, naam, hao maadui zako, hakika wataangamia; wote watendao maovu, watatawanyika!
10 Wewe umenipa nguvu kama nyati; umenimiminia mafuta ya kuburudisha.
11 Kwa macho nimeona maadui zangu wameshindwa; nimesikia kilio chao watendao maovu.
12 Waadilifu hustawi kama mitende; hukua kama mierezi ya Lebanoni!
13 Kama miti iliyopandwa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu, hustawi katika nyua za Mungu wetu;
14 huendelea kuzaa matunda hata uzeeni; daima wamejaa utomvu na wabichi;
15 wapate kutangaza kwamba Mwenyezi-Mungu ni mnyofu, Mwamba wangu, kwake hamna upotovu.

Generic placeholder image