118

Sala ya shukrani
1 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele.
2 Watu wa Israeli na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.”
3 Wazawa wa Aroni na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.”
4 Wote wamchao Mwenyezi-Mungu na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.”
5 Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu, naye akanisikia na kuniweka huru.
6 Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu; binadamu ataweza kunifanya nini?
7 Mwenyezi-Mungu yuko nami, kunisaidia; nami nitawaona maadui zangu wameshindwa.
8 Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kumtumainia mwanadamu.
9 Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia.
10 Mataifa yote yalinizingira, lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikayaangamiza!
11 Yalinizunguka kila upande, lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu, nikayaangamiza!
12 Yalinizunguka, mengi kama nyuki, lakini yakateketea kama kichaka motoni; kwa jina la Mwenyezi-Mungu niliyaangamiza!
13 Nilishambuliwa mno karibu nishindwe, lakini Mwenyezi-Mungu alinisaidia.
14 Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu; yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu.
15 Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu: “Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!
16 Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi! Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!”
17 Sitakufa, bali nitaishi, na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu.
18 Mwenyezi-Mungu ameniadhibu sana, lakini hakuniacha nife.
19 Nifungulie milango ya watu waadilifu, niingie na kumshukuru Mwenyezi-Mungu!
20 Huu ndio mlango wa Mwenyezi-Mungu, watu waadilifu watapitia humo.
21 Nakushukuru, ee Mungu kwa kunijibu; kwa sababu wewe ni wokovu wangu.
22 Jiwe walilokataa waashi, limekuwa jiwe kuu la msingi.
23 Hiyo ni kazi yake Mwenyezi-Mungu nayo ni ya ajabu sana kwetu.
24 Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi-Mungu; tushangilie na kufurahi.
25 Tafadhali utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu! Tafadhali utufanikishe, ee Mwenyezi-Mungu!
26 Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mwenyezi-Mungu! Twawabariki kutoka nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu
27 Mwenyezi-Mungu ni Mungu; yeye ametujalia mwanga wake Shikeni matawi ya sherehe, mkiandamana mpaka madhabahuni.
28 Wewe ni Mungu wangu, nami ninakushukuru; ninakutukuza, ee Mungu wangu.
29 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele.

Generic placeholder image