20

Kuomba ushindi
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni; jina la Mungu wa Yakobo likulinde.
2 Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake; akutegemeze kutoka mlima Siyoni.
3 Azikumbuke sadaka zako zote; azikubali tambiko zako za kuteketezwa.
4 Akujalie unayotamani moyoni mwako, aifanikishe mipango yako yote.
5 Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako; tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote!
6 Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa.
7 Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
8 Hao watajikwaa na kuanguka; lakini sisi tutainuka na kusimama imara.
9 Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu; utujibu wakati tunapokuomba.

Generic placeholder image