76

Mungu mshindi
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Asafu. Wimbo)
1 Mungu anajulikana katika Yuda; jina lake ni kuu katika Israeli.
2 Makao yake yamo huko Salemu; maskani yake huko Siyoni.
3 Huko alivunja mishale ya adui; alivunja ngao, panga na silaha za vita.
4 Wewe, ee Mungu, watukuka mno; umejaa fahari kuliko milima ya milele.
5 Wenye nguvu walipokonywa nyara zao, sasa wamelala usingizi wa kifo, mashujaa wa vita hawakuweza kutumia mikono yao.
6 Ulipowakemea, ee Mungu wa Yakobo, farasi na wapandafarasi walikufa ganzi.
7 Wewe, ee Mungu, ni wa kutisha mno! Nani awezaye kustahimili mbele yako ukikasirika?
8 Ulijulisha hukumu yako toka mbinguni; dunia iliogopa na kunyamaza;
9 wakati ulipoinuka kutekeleza hukumu, kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.
10 Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako; na waliookoka vitani watafanya sikukuu zako.
11 Mtimizieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ahadi zenu; enyi mlio karibu mpeni zawadi Mungu wa kutisha.
12 Yeye huzitoa roho za wakuu; huwatisha wafalme wa dunia.

Generic placeholder image