57
Kuomba msaada(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi alipomponyoka Shauli na kujificha pangoni) 1 Unihurumie, ee Mungu, unihurumie, maana kwako nakimbilia usalama. Kivulini mwa mabawa yako nitakimbilia usalama, hata hapo dhoruba ya maangamizi itakapopita. 2 Namlilia Mungu Mkuu, Mungu anikamilishiaye nia yake. 3 Atanipelekea msaada toka mbinguni na kuniokoa; atawaaibisha hao wanaonishambulia. Mungu atanionesha fadhili zake na uaminifu wake! 4 Mimi nimezungukwa na maadui, wenye uchu wa damu kama simba; meno yao ni kama mikuki na mishale, ndimi zao ni kama panga kali. 5 Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote! 6 Maadui wamenitegea wavu waninase, nami nasononeka kwa huzuni. Wamenichimbia shimo njiani mwangu, lakini wao wenyewe wametumbukia humo. 7 Niko thabiti moyoni, ee Mungu, naam, niko thabiti moyoni; nitaimba na kukushangilia! 8 Amka, ee nafsi yangu! Amkeni, enyi kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko! 9 Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa; nitakuimbia sifa kati ya mataifa. 10 Fadhili zako zaenea hata juu ya mbingu, uaminifu wako wafika hata mawinguni. 11 Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote!