63

Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
(Zaburi ya Daudi wakati alipokuwa katika jangwa la Yudea)
1 Ee Mungu, wewe u Mungu wangu, nami nakutafuta kwa moyo; roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu; nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji.
2 Nimetaka kukuona patakatifuni pako, niione nguvu yako na utukufu wako.
3 Fadhili zako ni bora kuliko maisha, nami nitakusifu kwa mdomo wangu.
4 Nitakushukuru maisha yangu yote; nitainua mikono yangu na kukuomba.
5 Roho yangu inafurahi kama kwa karamu na vinono; kwa shangwe nitaimba sifa zako.
6 Niwapo kitandani ninakukumbuka, usiku kucha ninakufikiria;
7 maana wewe umenisaidia daima. Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
8 Roho yangu inaambatana nawe kabisa, mkono wako wa kulia wanitegemeza.
9 Lakini hao wanaotaka kuyaangamiza maisha yangu, watatumbukia chini kwenye makao ya wafu.
10 Watauawa kwa upanga, watakuwa chakula cha mbweha.
11 Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu; wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu, lakini vinywa vya waongo vitafumbwa.

Generic placeholder image