43

Sala ya mkimbizi yaendelea
(Zaburi ya 42 yaendelea)
1 Onesha kuwa sina hatia ee Mungu; utetee kisa changu dhidi ya watu wabaya; uniokoe na watu waongo na waovu.
2 Nakimbilia usalama kwako ee Mungu; kwa nini umenitupilia mbali? Yanini niende huko na huko nikiomboleza kwa kudhulumiwa na adui yangu?
3 Upeleke mwanga na ukweli wako viniongoze, vinipeleke kwenye mlima wako mtakatifu, kwenye makao yako.
4 Hapo, ee Mungu, nitakwenda madhabahuni pako; nitakuja kwako, ee Mungu, furaha yangu kuu. Nitakusifu kwa zeze, ee Mungu, Mungu wangu.
5 Mbona ninahuzunika hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.

Generic placeholder image