28

Kuomba msaada
(Zaburi ya Daudi)
1 Nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu! Ewe mwamba wa usalama wangu usiniwie kama kiziwi, la sivyo kama usiponisikiliza, nitakuwa kama wale washukao shimoni kwa wafu.
2 Sikiliza sauti ya ombi langu, ninapokulilia unisaidie, ninapoinua mikono yangu kuelekea maskani yako takatifu.
3 Usinipatilize pamoja na watu wabaya, pamoja na watu watendao maovu: Watu wasemao na wenzao maneno ya amani, kumbe wamejaa uhasama moyoni.
4 Uwaadhibu kadiri ya matendo yao, kufuatana na maovu waliyotenda. Waadhibu kadiri ya matendo yao wenyewe; uwatendee yale wanayostahili.
5 Hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu; hawatambui mambo aliyoyafanya. Kwa sababu hiyo atawabomoa, wala hatawajenga tena upya.
6 Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, maana amesikiliza ombi langu.
7 Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
8 Mwenyezi-Mungu ni nguvu ya watu wake; yeye ni kimbilio la wokovu kwa mfalme wake mteule.
9 Ee Mungu, uwaokoe watu wako; uwabariki watu hao walio mali yako. Uwe mchungaji wao na kuwategemeza milele.

Generic placeholder image