58

Mungu hakimu wa mahakimu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi)
1 Enyi watawala, je, mwahukumu kwa haki kweli? Je, mnawahukumu watu kwa adili?
2 La! Nyinyi mwafikiria tu kutenda maovu; nyinyi wenyewe mwaeneza dhuluma nchini.
3 Waovu wamepotoka tangu kuzaliwa kwao, waongo hao, wamekosa tangu walipozaliwa.
4 Wana sumu kama sumu ya nyoka; viziwi kama joka lizibalo masikio,
5 ambalo halisikii hata sauti ya mlozi, au utenzi wa mganga stadi wa uchawi.
6 Ee Mungu, wavunje meno yao, yangoe, ee Mwenyezi-Mungu, meno ya simba hao.
7 Watoweke kama maji yanayodidimia mchangani, kama nyasi wakanyagwe na kunyauka,
8 watoweke kama konokono ayeyukavyo, kama mimba iliyoharibika isiyoona kamwe jua!
9 Kabla hawajatambua, wangolewe kama miiba, michongoma au magugu. Kwa hasira ya Mungu, wapeperushwe mbali, wakiwa bado hai.
10 Waadilifu watafurahi waonapo waovu wanaadhibiwa; watatembea katika damu ya watu wabaya.
11 Watu wote watasema: “Naam, waadilifu hupata tuzo! Hakika yuko Mungu anayeihukumu dunia!”

Generic placeholder image