12

Kuomba msaada
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Sheminithi. Zaburi ya Daudi)
1 Fanya haraka, ee Mwenyezi-Mungu! Watu wema wamekwisha; waaminifu wametoweka miongoni mwa watu.
2 Kila mmoja humdanganya mwenzake, husema kwa kudanganya na kwa moyo wa unafiki.
3 Ee Mwenyezi-Mungu uikomeshe hiyo midomo ya udanganyifu, na ndimi hizo zinazojigamba kupindukia.
4 Wao husema: “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo tunayo, nani awezaye kututawala?”
5 Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Kwa sababu maskini wanadhulumiwa, na wahitaji wanapiga kite, sasa naja, nami nitawapa usalama wanaoutazamia.”
6 Neno la Mwenyezi-Mungu ni safi, safi kama fedha iliyosafishwa katika tanuri, naam, kama fedha iliyosafishwa mara saba.
7 Utulinde, ee Mwenyezi-Mungu, utukinge daima na kizazi hiki kiovu.
8 Waovu wanazunguka kila mahali; upotovu unatukuzwa kati ya watu.

Generic placeholder image