141

Hatari za tamaa mbaya
(Zaburi ya Daudi)
1 Nakuita, ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia! Uisikilize sauti yangu wakati ninapokuita!
2 Sala yangu uipokee kama ubani; niinuapo mikono yangu kwako unikubali kama tambiko ya jioni.
3 Ee Mwenyezi-Mungu ukilinde kinywa changu, uweke ulinzi mlangoni mwa mdomo wangu.
4 Unikinge nisielekee kufanya mabaya, nisijishughulishe na matendo maovu; nisijiunge na watu watendao mabaya, wala nisishiriki kamwe karamu zao.
5 Afadhali mtu mwema anipige kunionya; lakini sikubali kamwe kusifiwa na wabaya, maana nasali daima dhidi ya maovu yao.
6 Wakuu wao watakapopondwa miambani, ndipo watatambua maneno yangu yalikuwa sawa.
7 Mifupa yao itatawanywa mdomoni pa Kuzimu kama kuni zilizopasuliwa vipandevipande!
8 Bali mimi nakutegemea, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; ninakimbilia usalama kwako, usiniache hatarini.
9 Unikinge na mitego waliyonitegea, uniepushe na matanzi ya hao watu waovu.
10 Waovu wanaswe katika mitego yao wenyewe, wakati mimi najiendea zangu salama.

Generic placeholder image