148

Ulimwengu wote umsifu Mungu
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka mbinguni, msifuni kutoka huko juu mbinguni.
2 Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni, enyi majeshi yake yote.
3 Msifuni, enyi jua na mwezi, msifuni, enyi nyota zote zingaazo.
4 Msifuni, enyi mbingu za juu, na maji yaliyo juu ya mbingu.
5 Vyote vilisifu jina la Mwenyezi-Mungu, maana yeye aliamuru, na vyote vikawa.
6 Yeye aliviweka mahali pao daima, kwa amri ambayo haiwezi kubatilishwa.
7 Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka duniani; enyi majoka ya baharini na vilindini, msifuni.
8 Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji, upepo wa tufani unaotimiza amri yake!
9 Msifuni enyi milima na vilima, miti ya matunda na misitu!
10 Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao, viumbe vitambaavyo na ndege wote!
11 Msifuni enyi wafalme na mataifa yote; viongozi na watawala wote duniani!
12 Msifuni enyi wavulana na wasichana; wazee wote na watoto pia!
13 Nyote lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, maana jina lake peke yake latukuka; utukufu wake wapita dunia na mbingu.
14 Amewapa watu wake nguvu; heshima kwa watu wote waaminifu, watu wa Israeli wapenzi wake. Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image