102

Sala katika taabu
(Sala ya mtu aliye katika shida na ambaye anamwekea Mwenyezi-Mungu malalamiko yake)
1 Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu, na kilio changu kikufikie.
2 Usijifiche mbali nami wakati wa taabu! Unitegee sikio lako, unijibu upesi wakati ninapokuomba!
3 Siku zangu zapita kama moshi; mifupa yangu yaungua kama katika tanuri.
4 Nimepondwa moyoni kama nyasi na kunyauka; sina hata hamu ya chakula.
5 Kutokana na kusononeka kwangu, nimebaki mifupa na ngozi.
6 Nimekuwa kama ndege wa jangwani; kama bundi kwenye mahame.
7 Ninalala macho wazi, kama ndege mkiwa juu ya paa.
8 Mchana kutwa maadui zangu wananisimanga, wanaonidhihaki hutumia jina langu kulaania.
9 Majivu yamekuwa chakula changu, machozi nayachanganya na kinywaji changu,
10 kwa sababu ya ghadhabu na hasira yako, maana umeniokota na kunitupilia mbali.
11 Maisha yangu ni kama kivuli cha jioni; ninanyauka kama nyasi.
12 Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele; jina lako lakumbukwa vizazi vyote.
13 Wewe utainuka na kuurehemu mji wa Siyoni; maana wakati umefika wa kuutendea mema; wakati wake uliopangwa umefika.
14 Watumishi wako wanauthamini sana, ujapokuwa magofu sasa; wanauonea huruma, ingawa umeharibika kabisa.
15 Mataifa yataliheshimu jina la Mwenyezi-Mungu; wafalme wote duniani wataogopa utukufu wake.
16 Mwenyezi-Mungu ataijenga upya Siyoni, na kuonekana alivyo mtukufu.
17 Ataikubali sala ya fukara; wala hatayakataa maombi yao.
18 Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vijavyo; watakaozaliwa baadaye wamsifu Mwenyezi-Mungu.
19 Kwamba aliangalia chini kutoka patakatifu pake juu, Mwenyezi-Mungu aliangalia dunia kutoka mbinguni,
20 akasikia lalamiko la wafungwa; akawaachilia huru waliohukumiwa kuuawa.
21 Hivyo watu watatangaza jina la Mwenyezi-Mungu huko Siyoni; sifa zake zitatangazwa huko Yerusalemu,
22 wakati mataifa yatakapokusanyika pamoja na falme zitakutana kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
23 Mungu amenipunguzia nguvu ningali kijana; ameyafupisha maisha yangu.
24 Ee Mungu wangu, usinichukue sasa wakati ningali bado kijana. Ee Mwenyezi-Mungu wewe wadumu milele.
25 Wewe uliiumba dunia zamani za kale, mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki; hizo zitachakaa kama vazi. Utazitupilia mbali kama nguo, nazo zitapotelea mbali.
27 Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayana mwisho.
28 Watoto wa watumishi wako watakaa salama; wazawa wao wataimarishwa mbele yako.

Generic placeholder image