11

Kumtumainia Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Kwake Mwenyezi-Mungu nakimbilia usalama; mnawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege, mpaka milimani,
2 maana waovu wanavuta pinde; wameweka mishale tayari juu ya uta, wawapige mshale watu wema gizani!
3 Kama misingi ikiharibiwa, mtu mwadilifu atafanya nini?”
4 Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu; kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu kiko mbinguni. Kwa macho yake huwachungulia wanadamu, na kujua kila kitu wanachofanya.
5 Mwenyezi-Mungu huwapima waadilifu na waovu; huwachukia kabisa watu wakatili.
6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto na madini ya kiberiti; upepo wa hari utakuwa ndio adhabu yao.
7 Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu na apenda uadilifu; watu wanyofu watakaa pamoja naye.

Generic placeholder image