86

Kuomba msaada
(Sala ya Daudi)
1 Unitegee sikio, ee Mwenyezi-Mungu, unijibu, maana mimi ni fukara na mnyonge.
2 Uyahifadhi maisha yangu maana mimi ni mchaji wako; uniokoe mimi mtumishi wako ninayekutegemea.
3 Wewe ni Mungu wangu; basi, unionee huruma, maana nakulilia mchana kutwa.
4 Uifurahishe roho yangu mimi mtumishi wako, maana sala zangu nazielekeza kwako ee Bwana.
5 Wewe, ee Bwana, u mwema na mwenye kusamehe; mwingi wa fadhili kwa wote wakuombao.
6 Ee Mwenyezi-Mungu, uitegee sikio sala yangu; ukisikie kilio cha ombi langu.
7 Siku za taabu nakuita, maana wewe waniitikia.
8 Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe; hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.
9 Mataifa yote uliyoyaumba, yatakuja kukuabudu, ee Bwana; yatatangaza ukuu wa jina lako.
10 Wewe ndiwe mkuu, wafanya maajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu.
11 Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu, nipate kuwa mwaminifu kwako; uongoze moyo wangu nikuheshimu.
12 Ee Bwana, Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitatangaza ukuu wa jina lako milele.
13 Fadhili zako kwangu ni nyingi mno! Umeniokoa kutoka chini kuzimu.
14 Ee Mungu, watu wenye kiburi wamenikabili; kundi la watu wakatili wanataka kuniua, wala hawakujali wewe hata kidogo.
15 Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa rehema na huruma; wewe ni mvumilivu, mwingi wa fadhili na uaminifu.
16 Unigeukie, unihurumie; unijalie nguvu yako mimi mtumishi wako, umwokoe mtoto wa mjakazi wako.
17 Unioneshe ishara ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, ili wale wanaonichukia waaibike, waonapo umenisaidia na kunifariji.

Generic placeholder image