KITABU CHA TATU
(Zaburi 73–89)

73

Haki itatawala
(Zaburi ya Asafu)
1 Hakika, Mungu ni mwema kwa watu wanyofu; ni mwema kwa walio safi moyoni.
2 Karibu sana ningejikwaa, kidogo tu ningeteleza;
3 maana niliwaonea wivu wenye kiburi, nilipoona wakosefu wakifanikiwa.
4 Maana hao hawapatwi na mateso; miili yao ina afya na wana nguvu.
5 Taabu za binadamu haziwapati hao; hawapati mateso kama watu wengine.
6 Kiburi kimekuwa mkufu wao shingoni, uhasama ni kama nguo yao.
7 Macho yao hufura kwa uovu; mioyo yao hububujika mipango mibaya.
8 Huwadhihaki wengine na kusema mabaya; hujivuna na kupanga kufanya uhasama.
9 Kwa vinywa vyao hutukana mbingu; kwa ndimi zao hujitapa duniani.
10 Hata watu wa Mungu wanawafuata, hawaoni kwao chochote kibaya na kusadiki kila wanachosema.
11 Wanasema: “Mungu hawezi kujua! Mungu Mkuu hataweza kugundua!”
12 Hivi ndivyo watu waovu walivyo; wana kila kitu na wanapata mali zaidi.
13 Je, nimetunza bure usafi moyoni, na kujilinda nisitende dhambi?
14 Mchana kutwa nimepata mapigo, kila asubuhi nimepata mateso.
15 Kama ningalisema hayo kama wao, ningalikuwa mhaini miongoni mwa watu wako.
16 Basi, nilijaribu kufikiria jambo hili, lakini lilikuwa gumu mno kwangu,
17 mpaka nilipoingia patakatifu pako. Ndipo nikatambua yatakayowapata waovu.
18 Kweli wewe wawaweka mahali penye utelezi; wawafanya waanguke na kuangamia.
19 Wanaangamizwa ghafla, na kufutiliwa mbali kwa vitisho.
20 Ee Bwana, uinukapo, wao hutoweka mara, kama ndoto wakati mtu anapoamka asubuhi.
21 Nilipoona uchungu moyoni na kuchomwa rohoni,
22 nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa kama mnyama mbele yako.
23 Hata hivyo niko daima nawe, ee Mungu! Wanishika mkono na kunitegemeza.
24 Wewe waniongoza kwa mashauri yako; mwishowe utanipokea kwenye utukufu.
25 Mbinguni, nani awezaye kunisaidia ila wewe? Na duniani hamna ninachotamani ila wewe!
26 Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
27 Anayejitenga nawe, hakika ataangamia. Anayekukana, utamwangamiza.
28 Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu, wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu. Nitatangaza mambo yote uliyotenda!

Generic placeholder image