50

Ibada ya kweli
(Zaburi ya Asafu)
1 Mungu wa nguvu Mwenyezi-Mungu, amenena, amewaita wakazi wa dunia, tokea mawio ya jua hadi machweo yake.
2 Kutoka Siyoni, mji mzuri mno, Mungu anajitokeza, akiangaza.
3 Mungu wetu anakuja, na sio kimyakimya: Moto uunguzao wamtangulia, na dhoruba kali yamzunguka.
4 Kutoka juu anaziita mbingu na dunia; zishuhudie akiwahukumu watu wake:
5 “Nikusanyieni waaminifu wangu, waliofanya agano nami kwa tambiko!”
6 Mbingu zatangaza uadilifu wa Mungu; kwamba Mungu mwenyewe ni hakimu.
7 “Sikilizeni watu wangu, ninachosema! Israeli, natoa ushahidi dhidi yako. Mimi ni Mungu! Mimi ni Mungu wako!
8 Sikukaripii kwa sababu ya tambiko zako; hujaacha kunitolea tambiko za kuteketeza.
9 Kwa kweli sina haja na fahali wa zizi lako, wala beberu wa mifugo yako;
10 maana wanyama wote porini ni mali yangu, na maelfu ya wanyama milimani ni wangu.
11 Ndege wote wa mwitu ni mali yangu, na viumbe vyote hai mashambani ni vyangu.
12 Kama ningeona njaa singekuambia wewe, maana ulimwengu na vyote vilivyomo ni vyangu.
13 Je, wadhani nala nyama ya fahali, au Kunywa damu ya mbuzi?
14 Shukrani iwe ndio tambiko yako kwa Mungu mtimizie Mungu Aliye Juu ahadi zako.
15 Uniite wakati wa taabu, nami nitakuokoa, nawe utaniheshimu.”
16 Lakini Mungu amwambia mtu mwovu: “Ya nini kuzitajataja tu sheria zangu? Kwa nini unasemasema juu ya agano langu?
17 Wewe wachukia kuwa na nidhamu, na maneno yangu hupendi kuyafuata.
18 Ukimwona mwizi unaandamana naye, na wazinzi unashirikiana nao.
19 Uko tayari daima kunena mabaya; kazi ya ulimi wako ni kutunga uongo.
20 Wakaa kitako kumsengenya binadamu mwenzako, naam, kumchongea ndugu yako mwenyewe.
21 Umefanya hayo yote nami nimenyamaa. Je, wadhani kweli mimi ni kama wewe? Lakini sasa ninakukaripia, ninakugombeza waziwazi.
22 “Fikirini vizuri jambo hili, enyi msionijali, la sivyo nitawaangamizeni, wala hapatakuwa na wa kuwaokoeni.
23 Anayenipa shukrani kama tambiko yake, huyo ndiye anayeniheshimu; yeyote anayedumu katika njia yangu, huyo ndiye nitakayemwokoa.”

Generic placeholder image