109

Lalamiko la mtu taabuni
(Kwa Mwimbishaji. Wimbo wa Daudi)
1 Usinyamaze, ee Mungu ninayekusifu!
2 Watu waovu na wadanganyifu wanishambulia, wanasema uongo dhidi yangu.
3 Wanasema maovu juu yangu, na kunishambulia bila kisa.
4 Ingawa niliwapenda, walinishtaki, hata hivyo niliwaombea dua.
5 Wananilipa uovu kwa wema wangu, na chuki kwa mapendo yangu.
6 Umweke hakimu mbaya dhidi ya adui yangu; na mshtaki wake ampeleke mahakamani.
7 Anapohukumiwa apatikane na hatia; lalamiko lake lihesabiwe kuwa kosa jingine.
8 Siku za maisha yake ziwe chache, mtu mwingine na achukue kazi yake!
9 Watoto wake wawe yatima, na mke wake awe mjane!
10 Watoto wake watangetange na kuombaomba; wafukuzwe katika magofu ya nyumba zao!
11 Anayemdai kitu amnyanganye mali yake yote; na wageni wanyakue mapato ya jasho lake!
12 Pasiwe na mtu wa kumwonea huruma, au Kuwatunza watoto wake yatima!
13 Wazawa wake wote wafe; jina lake lisahauliwe katika kizazi kijacho!
14 Mwenyezi-Mungu aukumbuke uovu wa wazee wake, dhambi za mama yake zisifutwe kamwe!
15 Mwenyezi-Mungu azikumbuke dhambi zao daima; lakini wao wenyewe wasahauliwe duniani.
16 Mwovu huyo hakujali kabisa kuwa na huruma, ila aliwadhulumu maskini na fukara, kadhalika na watu wanyonge mpaka kifo.
17 Yeye alipenda kulaani watu, laana na impate yeye mwenyewe. Hakuwatakia wengine baraka, basi, asipate baraka yeye mwenyewe.
18 Kwake kulaani ni kama kuvaa nguo, basi, laana hizo zimloweshe kama maji, zimwingie mifupani mwake kama mafuta.
19 Laana zimfunike kama nguo, zimzunguke daima kama ukanda.
20 Mwenyezi-Mungu awalipe hayo hao watu wanaonishtaki, naam hao wanaosema mabaya dhidi yangu.
21 Lakini ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, unitendee kadiri ya hisani yako; uniokoe, kwa sababu ya wema wa fadhili zako!
22 Mimi ni maskini na fukara; nimejeruhiwa mpaka moyoni mwangu.
23 Natoweka kama kivuli cha jioni; nimepeperushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamenyongonyea kwa mfungo; nimebaki mifupa na ngozi.
25 Nimekuwa dhihaka tupu kwa watu; wanionapo hutikisa vichwa vyao kwa dharau.
26 Unisaidie, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; uniokoe kadiri ya fadhili zako.
27 Waoneshe watu kuwa ndiwe uliyetenda hayo, wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe uliyefanya hivyo.
28 Waache walaani, lakini wewe unibariki; wanaonishambulia waaibike, nami mtumishi wako nifurahi.
29 Maadui zangu na wavishwe fedheha; wajifunike aibu yao kama blanketi.
30 Nitamshukuru sana Mwenyezi-Mungu kwa sauti; nitamsifu kati ya kundi kubwa la watu,
31 kwa maana yeye humtetea maskini, humwokoa wakati anapohukumiwa.

Generic placeholder image