83

Sala dhidi ya adui za Israeli
(Zaburi ya Asafu. Wimbo)
1 Ee Mungu, usikae kimya! Usinyamaze ee Mungu, wala usitulie!
2 Tazama! Maadui zako wanafanya ghasia; wanaokuchukia wanainua vichwa kwa kiburi.
3 Wanapanga kwa hila kuwadhuru watu wako; wanashauriana dhidi ya hao unaowalinda.
4 Wanasema: “Njoni tuliangamize taifa lao, jina la Israeli lisikumbukwe tena.”
5 Naam, wanakubaliana kwa moyo mmoja, wanakula kiapo dhidi yako:
6 Watu wa Edomu na Waishmaeli, Wamoabu na watu wa Hagari;
7 watu wa Gebali, Amoni na Amaleki, watu wa Filistia na wakazi wa Tiro.
8 Hata Ashuru imeshirikiana nao, imewaunga mkono wazawa wa Loti!
9 Uwatende ulivyowatenda watu wa Midiani, ulivyowatenda Sisera na Yabini mtoni Kishoni,
10 watu uliowaangamiza kule Endori, wakawa takataka juu ya nchi.
11 Uwatende wakuu wao kama Orebu na Zeebu; watawala wao wote kama Zeba na Zalmuna,
12 ambao walisema: “Tutajitekea nchi ya Mungu.”
13 Ee Mungu wangu, uwafanye kama vumbi; kama makapi yapeperushwayo na upepo.
14 Kama vile moto unavyoteketeza msitu, na miali ya moto inavyounguza milima,
15 uwakimbize hao kwa tufani yako, na kuwatisha kwa kimbunga chako!
16 Uzijaze nyuso zao fedheha, wapate kukutafuta, ee Mwenyezi-Mungu.
17 Waone fedheha na kuhangaika milele, waangamie kwa aibu kabisa.
18 Wajue kwamba wewe peke yako ambaye jina lako ni Mwenyezi-Mungu, ndiwe Mungu Mkuu juu ya dunia yote.

Generic placeholder image