45

Utenzi wa kumsifu mfalme
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Utenzi wa Wakorahi; utenzi wa mapenzi)
1 Moyo wangu umejaa mawazo mema: Namtungia mfalme shairi langu, ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi.
2 Wewe u mzuri kuliko wanadamu wote, maneno yako ni fadhili tupu. Kwa hiyo Mungu amekubariki milele.
3 Jifunge upanga wako, ewe shujaa! Wewe ni mtukufu na mwenye fahari.
4 Songa mbele kwa utukufu upate ushindi, utetee ukweli na kulinda haki. Mkono wako utende mambo makuu.
5 Mishale yako ni mikali, hupenya mioyo ya maadui za mfalme; nayo mataifa huanguka chini yako.
6 Kiti chako cha enzi ni imara, chadumu milele kama cha Mungu. Wewe watawala watu wako kwa haki.
7 Wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua, na kukupa furaha kuliko wenzako.
8 Mavazi yako yanukia marashi na udi, wanamuziki wakuimbia katika majumba ya pembe za ndovu.
9 Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki, naye malkia amesimama kulia kwako, amevaa mapambo ya dhahabu safi ya Ofiri.
10 Sikiliza binti, ufikirie! Tega sikio lako: Sahau sasa watu wako na jamaa zako.
11 Uzuri wako wamvutia mfalme; yeye ni bwana wako, lazima umtii.
12 Watu wa Tiro watakuletea zawadi; matajiri watataka upendeleo wako.
13 Binti mfalme anaingia mzuri kabisa! Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.
14 Akiwa amevalia vazi la rangi nyingi, anaongozwa kwa mfalme, akisindikizwa na wasichana wenzake; nao pia wanapelekwa kwa mfalme.
15 Kwa furaha na shangwe wanafika huko, na kuingia katika jumba la mfalme.
16 Ee mfalme, utapata watoto wengi watakaotawala mahali pa wazee wako; utawafanya watawale duniani kote.
17 Nitalifanya jina lako litukuzwe katika vizazi vyote, nayo mataifa yatakusifu daima na milele.

Generic placeholder image