60

Ushindi baada ya kushindwa
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Shushani Edut. Utenzi wa Daudi wa kufundisha, wakati alipopigana na Waaramu kutoka Naharaimu na Zoba, Yoabu aliporudi nyuma na kuwaua Waedomu 12,000 katika Bonde la Chumvi)
1 Ee Mungu, umetutupa na kutuponda, umewaka hasira, tafadhali uturudishie nguvu.
2 Umeitetemesha nchi na kuipasua; uzibe nyufa zake kwani inabomoka.
3 Umewatwika watu wako mateso; tunayumbayumba kama waliolewa divai.
4 Uwape ishara wale wanaokuheshimu, wapate kuuepa mshale.
5 Uwasalimishe hao watu uwapendao; utuokoe kwa mkono wako, na kutusikiliza.
6 Mungu amesema kutoka patakatifu pake “Sasa nitaigawa Shekemu kwa shangwe, Bonde la Sukothi nitalipima sehemusehemu.
7 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni kofia yangu ya chuma, na Yuda ni fimbo yangu ya enzi.
8 Moabu ni kama bakuli langu la kunawia, kiatu changu nitaitupia Edomu kuimiliki. Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia.”
9 Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wa ngome? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?
10 Je, umetuacha kabisa, ee Mungu? Wewe huendi tena na majeshi yetu!
11 Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu, maana msaada wa binadamu haufai kitu.
12 Mungu akiwa upande wetu tutashinda, yeye atawaponda maadui zetu.

Generic placeholder image