25

Kumwomba Mungu uongozi na ulinzi
(Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu!
2 Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu, usiniache niaibike; adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.
3 Usimwache anayekutumainia apate aibu; lakini waaibike wote wanaokuasi kwa makusudi.
4 Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu; unifundishe nifuate unayotaka.
5 Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha, kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu; ninakutegemea wewe kila siku.
6 Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu; uzikumbuke na fadhili zako kuu, ambazo zimekuwako tangu kale.
7 Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu; unikumbuke kadiri ya fadhili zako, kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
8 Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia.
9 Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu; naam, huwafundisha hao njia yake.
10 Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu, kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.
11 Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, unisamehe kosa langu kwani ni kubwa.
12 Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata.
13 Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima, na wazawa wake watamiliki nchi.
14 Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao; yeye huwajulisha hao agano lake.
15 Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima; yeye atainasua miguu yangu mtegoni.
16 Unielekee, ee Mungu, unionee huruma, maana mimi ni mpweke na mnyonge.
17 Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu; unitoe katika mashaka yangu.
18 Uangalie mateso yangu na dhiki yangu; unisamehe dhambi zangu zote.
19 Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu; ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili.
20 Uyalinde maisha yangu, uniokoe; nakimbilia usalama kwako, usikubali niaibike.
21 Wema na uadilifu vinihifadhi, maana ninakutumainia wewe.
22 Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli; uwaokoe katika taabu zao zote.

Generic placeholder image