26

Sala ya mtu mwema
(Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, unitetee, maana nimeishi bila hatia, nimekutumainia wewe bila kusita.
2 Unijaribu, ee Mwenyezi-Mungu, na kunipima; uchunguze moyo wangu na akili zangu.
3 Fadhili zako ziko mbele ya macho yangu, ninaishi kutokana na uaminifu wako.
4 Sijumuiki na watu wapotovu; sishirikiani na watu wanafiki.
5 Nachukia mikutano ya wabaya; wala sitajumuika na waovu.
6 Nanawa mikono yangu kuonesha sina hatia, na kuizunguka madhabahu yako, ee Mwenyezi-Mungu,
7 nikiimba wimbo wa shukrani, na kusimulia matendo yako yote ya ajabu.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, napenda makao yako, mahali unapokaa utukufu wako.
9 Usiniangamize pamoja na wenye dhambi, wala usinitupe pamoja na wauaji,
10 watu ambao matendo yao ni maovu daima, watu ambao wamejaa rushwa.
11 Lakini mimi ninaishi kwa unyofu; unihurumie na kunikomboa.
12 Mimi nimesimama mahali palipo imara; nitamsifu Mwenyezi-Mungu katika kusanyiko kubwa.

Generic placeholder image